Huduma ya Afya kuboreshwa kwa wanachama wa CHF Karagwe
Na. Innocent Mwalo, KARAGWE.
Kikao cha Kamati ya Elimu,Afya na Maji kilichoketi mnamo tarehe 11/07/2017 katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya Karagwe chini ya Mwenyekiti wake Mh. Charles Beichumila kimeazimia kwa kauli moja kuboreshwa kwa huduma za afya kwa wananchi ambao ni wanachama wa mfuko wa Bima ya Afya (CHF) wilayani Karagwe.
Kauli hii ilikuja kupitia kikao hicho kilichokuwa kikifanya shughuli ya tathmini ya utekelezaji na utendaji wa shughuli za Idara na Vitengo vya Halmashauri ambavyo vinaingia kwenye Kamati hii kwa robo ya nne ya mwaka wa Fedha 2016/2017 lakini pia kilikuwa ndio kikao cha kufunga mwaka.
Awali, mwenyekiti wa Halmashauri hii, Mh. Wallace Mashanda licha ya kuwapongeza wahudumu wa afya wilayani hapa kwa kazi yao nzuri wanayofanya licha ya changamoto yao ya uhaba unaowakumba watumishi wa kada hii, aliagiza kupitia kwa Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Libamba Sobo kuhakikisha wananchi wenye kadi ya Bima ya Afya ya Mfuko wa Bima hiyo (CHF) kupata huduma inayostahili kwani kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi hao wanashindwa kuhudumiwa vizuri kwa kikwazo cha kuwa na Bima ya Afya.
Kauli hiyo iliungwa mkono na wajumbe wote wa mkutano huku ushauri ukitolewa kupitia kikao hicho wa Idara ya Afya wilayani hapa kufanyia kazi changamoto hiyo.
Jambo jingine lililoibuka katika kikao hicho lilikuwa kuridhia kwa mikakati kadhaa ya kuhakikisha huduma ya matibabu bure kwa wazee inaendelea kutolewa na kwa pamoja iliazimiwa kuwa na mkakati wa kuanzisha/kufufua mabaraza ya wazee kuanzia ngazi ya kijiji hadi kata ili kurahisha upatikanaji wa taarifa za wazee.
Mikakati mingine ilikuwa ni kwamba kila kituo kinunue kamera kwa ajili ya kurahisha zoezi la kupiga picha za matibabu ya wazee.
Kamati ya Elimu, Afya na Maji huundwa na Idara na Vitengo vifuatavyo; Idara ya Afya, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Idara ya Elimu Msingi, Idara ya Elimu ya Sekondari, Idara ya Maji vijijini, Idara ya Maji Mjini, Idara ya Mazingira na Taka ngumu pamoja na ile inayohusu Chuo cha Ufundi cha Wilaya (KDVTC) hufanyika kila baada ya miezi mitatu ili kujadili taarifa mbalimbali za Idara hizo na kutoa mapendekezo na maelekezo kwa wataalam wa Halmashauri na kimsingi ajenda za kikao hiki ambacho ni moja ya kamati za Halamshauri huwa ni moja kati ya ajenda zinazowasilishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani (Full Council)
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.