Halmashauri ya Wilaya Karagwe Yatoa Mikopo kwa Wanawake na Vijana
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Halmashauri ya Wilaya Karagwe, mnamo tarehe 23/10/2017 ilikabidhi hundi yenye thamani ya shilingi Milioni kumi na nane (18,000,000/=) kwa ajili ya mfuko wa vikundi sita vya vijana na wanawake ambapo kila kikundi kilipewa kiasi cha sh. 3,000,000/= ikiwa ni mkopo kwa ajili ya kuyainua makundi hayo kiuchumi kama ilivyoelekezwa na serikali kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015- 2020 inayoziagiza Halmashauri za Wilaya kote nchini kutenga kiasi cha asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa makundi hayo.
Vikundi hivyo vinanavyopata mkopo katika robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2017/2018 vinatoka katika kata sita za Halmashauri ya Wilaya hii huku utaratibu huu ukitajwa kuendelea katika kata nyingine 17 zilizobaki katika kipindi cha mwaka huu wa Fedha.
Shughuli ya makabidhiano ya fedha hizo zilifanyika katika viunga vya ofisi ya Mkuu wa Wilaya Karagwe vikihudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama na serikali wilayani hapa wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Karagwe Mh. Godfrey Mheluka ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye pia aliambatana na wajumbe wote wa Kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya hii.
Wengine katika hafla hiyo walikuwa ni waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya wilaya Karagwe wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mh. Wallace Mashanda.
Pia walikuwepo viongozi wa vyama vya siasa kikiwemo chama tawala, CCM waliokuwa wakiongozwa na Mwenyekiti wao wa CCM Wilaya ndugu Robinson Mutafungwa.
Kwa upande wa watumishi wa Halmashauri ya wilaya Karagwe, wakuu wa Idara na Vitengo, pamoja na watumishi wote wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ndugu Ashura Kajuna walihudhuria hafla hiyo lakini pia wananchi wengi wa Karagwe walishiriki na kushuhudia tukio hilo muhimu .
Mapema katika taarifa yake kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, ndugu Adeodata Augustine Peter, ambayo kimsingi ndio Idara yenye jukumu la uratibu wa utoaji wa mikopo kwa vikundi katika Halmashauri alivitaja vikundi hivyo ambapo kila kikundi kilipewa mkopo wa kiasi cha shilingi 3,000,000/= kila kimoja, huku kila kikundi kikitakiwa kurejesha kiasi cha shilingi 356,667/= kwa mwezi (ikiwa ni riba ya asilimia 07 yenye thamani ya sh.210,000/=) huku tarehe ya kukamilisha urejeshwaji wa mkopo huo ikitajwa kuwa 20/10/2018.
Vikundi hivyo vilivyotajwa kupita taarifa ya Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii vilikuwa ni Umoja wa Vijana Wajasiliamali Kishoju chenye wananchama 10 kutoka katika kata ya Kihanga, Kikundi cha wanawake cha Mkombozi chenye wanachama 21 kutoka kata ya Kanoni na kikundi cha vijana cha Youth Carpentry Design Centre kilichopo kata ya Nyashozi na chenye wanachama 10.
Vikundi vingine vilikuwa ni kikundi cha wanawake na vijana cha Saidiana kutoka kata ya Igurwa chenye Idadi ya wanachama 18, kikundi cha wanawake Vicoba cha Ngozi “A” chenye wanachama 30 kutoka kata ya Nyabiyonza na kingine kilikuwa ni kikundi cha vijana cha Matumaini chenye wanachama 16 kutoka katika kata ya Bugene.
“Awali ya yote napenda kuwapongeza kwa kuweza kupata nafasi ya kunufaika na mkopo huu mlioupata kutoka katika mfuko wa wanawake na vijana wa Halmashauri; hii ni bahati kubwa kwenu kwani wahitaji ni wengi ila uwezo wa Halmashauri ni mdogo kuweza kuwahudumia wahitaji wote kwa wakati mmoja kwani wapo wahitaji/ vikundi zaidi ya 1080,” alisema ndugu Adeodata katika taarifa yake kwa mgeni rasmi.
Taarifa hiyo ilisisitiza mambo muhimu ambayo wakopeswaji hao wanayopaswa kuzingatia baada ya kuchukua mkopo huu kuwa ni kama vile kuhakikisha mkopo huu unatumika kwa malengo yaliyopangwa na kwa kuzingatia kanuni na taratibu walizojiwekea bila kutawaliwa na ubinafsi wala upendeleo.
“Vile vikundi vya kuweka na kukopa vihakikishe vinasimamia taratibu mlizojiwekea zinazingatiwa kwa maana kwamba akopeshwe mtu ambaye ana sifa za kukopesheka na shughuli anayoifanya ifahamike na ikiwezekana viongozi wajiridhishe kabla ya kumpa mkopo,” alisema ndugu Adeodata kupitia taarifa hiyo.
Mambo mengine ni kwamba kwa vikundi vyenye miradi mingine vihakikishe fedha zote zinaingizwa katika shughuli za miradi si vinginevyo taarifa ya mapato na matumizi ifahamike kwa wanakikundi wote.
“Hakikisha mnakaa vikao kwa ajili ya kujadili maendeleo ya mradi ili kama kuna tatizo basi litafutiwe ufumbuzi kabla mradi haujaathirika zaidi,” ilinukuliwa kupitia taarifa hiyo.
“Hakikisheni marejesho yanafanyika kila mwezi kwa mjibu wa mkataba/maelekezo. Mkopo huu unakopeshwa kwa riba ya asilimia 7, utaanza kurejeshwa kila tarehe 20 ya kila mwezi kuanzia mwezi January 2018 na marejesho haya yanatakiwa kukamilika tarehe 20/09/2018 na hii ni kutokana na kuwa baada ya kuchukua mkopo mtapewa miezi mitatu ya neema kwa ajili ya kuwawezesha kuanza kuzalisha na kwa hivyo basi Mkopo pamoja na riba ni kiasi cha Tsh 3,210,000 hivyo kila mwezi mtarejesha tsh 357,000/= isipokuwa mwezi wa mwisho zitarejeshwa 354,000/,” aliendelea kusisitizwa kupitia taarifa hiyo.
“Kila baada ya miezi mitatu kikundi kiwasilishe taarifa ya maendeleo ya kikundi inayoonyesha mafanikio na changamoto za kikundi( mmundo wa .Mwisho lakini siyo kwa umuhimu, kikundikinatakiwa kioneshe matarajio yake ya baadae,” aliendelea kusisitiza ndugu Adeodata.
Naye Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Mheluka huku akipongeza jitihada hizo za utoaji wa mikopo aliiomba ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kutokuvipeleka mahakamani vikundi vilivyoshindwa kurejesha mikopo hiyo badala yake kabla ya kufikia uamuzi huo ni vizuri ofisi yake ikashirikishwa ili kuweza kuingilia kati.
“Mnaweza kuwapeleka mahakamani na mkatumia gharama kubwa wakati tungeweza kukaa chini na kikundi kinachodaiwa ili kuona nini changamoto,’’ alisema Mh. Mheluka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Karagwe, Mh. Mashanda aliungana na mkuu wa wilaya juu ya wazo lake la kukaa na Halmashauri na kujadilina na vikundi vinavyochelewa kufanya urejeshaji wa mikopo hiyo huku akitoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa ujumla kuhakikisha mikopo itakayotolewa kwenye mgawo mwingine kuliweka kundi jingine la walemavu ili nao waweze kunufaika na mikopo hiyo sambamba na makundi ya vijana na wanawake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM, ndugu Mutafungwa alisema ni lazima Halmashauri ya Wilaya iendelee kutenga fedha hicho kwani CCM iliahidi kutoa mikopo hiyo huku akiwashukuru baadhi ya madiwani wa vyama vya upinzani waliohudhuria hafla akilitaja kitengo hicho kuwa ni cha msingi sana kwa mstakabali wa maendeleo ya wilaya ya Karagwe.
Wakati huo huo SACCOS ya wanawake Karagwe (KAWOSA) imefika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Karagwe ikiwa na makombe mawili moja likiwa la kitaifa na jingine la kimkoa.
Uongozi wa KAWOSA ulifika ofisini kwa Mkuu wa wilaya kwa ajili ya kumshukuru kiongozi huyo kutokana na ushirikiano anaowapa hali iliyepelekea kupata kombe la kitaifa lililotolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa alilolitoa kwa KAWOSA mjini Dodoma mnamo tarehe 19/10/2017 kwa KAWOSA kuwa ni miongoni mwa SACCOS bora zinazofanya vizuri hapa nchini.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.