KITONKA: HALMASHAURI ITAENDELEA KUFANYA KAZI NA WADAU WA MAENDELEO.
Na, Geofrey A.Kazaula
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Ndg, Godwin M.Kitonka amesisitiza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe itaendelea kufanya kazi na wadau wa maendeleo ili kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Hayo yamejiri wakati Kiongozi huyo akifungua kikao cha Kamati ya Lishe ya Wilaya kilicholenga kuweka mikakati juu ya kukabiliana na tatizo la udumavu na lishe duni katika Wilaya ya Karagwe .
Ameeleza kuwa kazi hiyo ya kutoa elimu juu ya lishe inapaswa kutiliwa mkazo kwani Mkoa wa Kagera ni moja wapo ya mikoa yenye tatizo la udumavu.
‘‘ Kamati hii inapaswa kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu juu ya lishe bora kwa wananchi kwani Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye tatizo la udumavu’’ alieleza kiongozi huyo.
Alifafanua kuwa tatizo la udumavu lipo katika Mkoa wa Kagera na tatizo hilo linasababishwa kwa kiasi kikubwa na elimu ndogo juu ya lishe kwani watu hawajui nini wale , kwa wakati gani na umri upi wakula chakula fulani au kutokula.
‘’ Ukiuangalia Mkoa wa Kagera ni Mkoa uliojaliwa kuwa na vyakula vingi sana tena vya kila aina, karibu kila kitu kinapatikana katika Mkoa huu ila tatizo watu hawajui namna ya kutumia vyakula hivi jambo ambalo Kamati ya lishe inapaswa kulitilia mkazo hasa kuhakikisha watu wanapewa elimu’’ alieleza kiongozi huyo.
Aliagiza kuwa Idara ya Afya kupitia wataalam wake wa lishe na wadau wa maendeleo iandae vipeperushi vitakavyo waelekeza wananchi juu ya namna bora ya kula kwa kufafanua umri wa mtu na aina ya chakula anachopaswa kula kwa wingi pia muda sahihi wa kula aina fulani ya chakula.
Kwa upande wake Afisa lishe kutoka shirika la IMA World Health anayefanya kazi katika mradi wa mtoto mwelevu Bi. Idda Katigula alifafanua kuwa Shirika hilo litaendelea kusaidia katika utoaji wa elimu ya lishe ili kupambana na tatizo la udumavu.
‘’Iandaliwe taarifa ya watoto wenye uzito pungufu kwa kila Kata ili shirika liweze kuandaa Program ya kuhakikisha watoto hao wanasaidiwa kwa kila Kata’’ alifafanua Afisa huyo .
Aliongeza kuwa lengo la Shirika hilo ni kuhakikisha Afya ya watoto na Afya ya jamii kwa ujumla inaboreshwa ili kuwa na maendeleo endelevu.
Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye tatizo la udumavu ambapo Serikali Wilayani Karagwe kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo iko katika uchukuaji wa hatua za kupambana na tatizo hilo kwa kutoa elimu juu ya lishe kwa wananchi wake.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.