Elimu Yatolewa Juu ya Matumizi Bora ya Choo na Unawaji Mikono.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Katika harakati za kuungana na mataifa mengine duniani katika maadhimisho ya siku ya choo na unawaji wa mikono ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Novemba 19 ili kuitikia agizo lililotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wananchi wilayani Karagwe wamejitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kibogoizi, kata ya Ihembe kwa ajili ya sherehe hizo zilizokuwa na kauli mbiu ya “Dhibiti Maji Taka Tumia Choo Bora”
Mapema Novemba 19, 2017, mgeni rasmi, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hii, Mh. Nyangele Makunenge aliwasili katika maeneo hayo na kupokelewa na wataalam kadhaa kutoka Halmashauri ya Wilaya, zaidi wakiwa watumishi wa Idara ya Afya.
Katika mapokezi hayo alikuwepo Mtendaji wa kata hiyo ndugu Godian Msimba aliyeshirikiana na ndugu Josephat Nkebukwa aliyekuwa Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Afisa Afya wa wilaya ndugu Beatrice Laurent, mratibu wa mfuko wa Bima ya Afya ndugu Moses Aligawesa, Afisa Lishe ndugu Selemani Hamisi na Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii ndugu Mmasa Mmasa.
Wengine waliokuwa katika mapokezi hayo ni Afisa Utamaduni wa wilaya ndugu Aloyce Mujungu, mratibu wa Huduma ya Mama na Mtoto ndugu Claudia Nkuba, msaidizi katika ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ndugu Imelda Apolo na waandishi wa habari wa hapa wilayani Karagwe.
Baada ya mapokezi hayo, yalifanyika matumbuizo ya nyimbo, igizo na ngoma kutoka kwa wanafunzi na wasanii mbalimbali walionekana kukonga sana nyoyo za wananchi walikusanyika kwa ajili ya shamrashamra hizo.
Awali ndugu Beatrice Laurent alisoma risala kwa mgeni rasmi ambapo pamoja na mambo mengine alimweleza mgeni kiongozi huyo kwamba maadhimisho ya siku ya choo na unawaji wa mikono hutanguliwa na wiki ya uhamasishaji ambayo huanza kila Novemba 13 ya kila mwaka.
“Kwa mwaka huu ujumbe huo uliweza kutolewa kupitia vyombo vya habari pamoja na vituo vya tiba kila siku kabla ya kuanza kwa shughuli za kawaida za kazi kwa siku”, alisema ndugu Beatrice.
”Pamoja na kuhimiza jamii nzima ya Wilaya ya Karagwe juu ya ujenzi na matumizi ya choo bora na unawaji wa mikono kwa kutumia kibuyu chirizi ambapo serikali iliweka mkakati wa makusudi wa kuhakikisha vitongoji vinafikiwa na wataalam ili kuwapa Elimu hiyo”, alinukuliwa ndugu Beatrice Laurent kupitia taarifa hiyo.
Ndugu Beatrice aliendela kugusia kwamba mkakati huo Kampeni ya Afya na usafi wa mazingira ulioanza mwaka 2012 ambapo hadi sasa umeshafika kwenye kata 15 ambazo ni Kanoni, Igurwa, Kiruruma, Kamagambo, Nyabiyonza, Kibondo, Nyakabanga, Nyakakika, Bweranyange, Nyaishozi, Ihembe, Rugu, Nyakasimbi, Chonyonyo na Rugera.
“Tunatajia hadi mwezi Desemba kuongezeka kwa Kata ya Kihanga na hivyo tutakuwa tumebakiza kata saba lengo likiwa kuhakisha kila kaya ina choo chenye sifa za kuwa choo bora ambacho ni shimo lisilopungua urefu wa futi 12, sakafu inayosafishika, ukuta imara, paa iliyoezekwa na mlango uliofungwa (unaotunza siri) na kunawa mikono kwa kutumia kibuyu chirizi baada ya kutoka chooni na hii inatakiwa iwe tabia ya kudumu kwa manufaa ya jamii ya sasa na baadae”, alisema ndugu Beatrice.
Huku akirejea baadhi ya takwimu, ndugu Beatrice alianisha kwamba mwaka 2011 kabla ya kampeni hii, wilaya ya Karagwe na Kyerwa zilikuwa na vyoo bora kwa 48%, 29% walikuwa na vyoo visivyokuwa bora na 23% hawakuwa na vyoo kabisa huku akibainisha kwamba hali imekuwa bora zaidi kwani mpaka kufikia Septemba 2017 kaya zenye vyoo ni 96.8% huku vyoo bora ikiwa 78.1% na kaya ambazo hazina vyoo bora ni 3.2%
Aidha, ndugu Beatrice aliweza kuzitaja baadhi ya Taasisi ambazo vyoo vimekarabatiwa kuwa ni shule za msingi Kigarama, Rwambaizi, Kanoni, Ahamlama, Ahakanya na Bwera huku akieleza kwamba kila shule imeweza kujenga sehemu ya kukojoa wavulana ikiwa ni mradi wa kampeni ya Usafi na usafi wa mazingira kwa kushirikiana na vijiji husika.
“Pia katika kampeni hiyo shule ya msingi Rwentuhe na Nyabweziga wamepewa Elimu kuhusu Afya na usafi wa mazingira”, alisema ndugu Beatrice kupitia taarifa hiyo.
Naye mgeni rasmi, Mh. Nyangele Makunenge katika hotuba yake aliwaagiza wananchi kote wilayani Karagwe kutelekeza maagizo yanayotolewa na wataalam wa Idara ya Afya kuhusu matumizi bora ya choo na unawaji wa mikono.
“Napenda kuiasa jamii kuhudhuria mikutano ya Afya ambayo ndiyo inaweza kusaidia kupunguza magonjwa yanayozuilika kwa kubadili tabia na hii inaweza kusaidia kutokomezwa kwa magonjwa ya minyoo, homa ya matumbo, kuhara na kuhara damu, kipindupindu na mengine kama hayo yanayotokana na kula kinyesi cha binadamu”, alisisitiza Mh. Nyangele.
Katika hatua nyingine mgeni rasmi aliweza kukabidhi zawadi ya kiasi cha Sh. 30,000/= kwa mzee Swedi Nkurunungi ili aweze kujenga choo bora kutokana na mzee huyo kukumbwa na maradhi yanayomfanya kutokujenga choo bora lakini akijitahidi kujenga choo; zawadi hiyo ilipokelewa na binti yake aitwaye Zidina Swedi.
Pia mgeni rasmi alipata kufika kwenye eneo la kibuyu chirizi ambapo ndugu Beatrice alitumia muda huo kupitia mgeni rasmi kutoa Elimu kwa wananchi waliokuwa wamekusanyika kwenye maeneo hayo kutoa Elimu ya matumizi ya kibuyu chirizi.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibogoizi ndugu Joktani Kbengo, Mwenyekiti wa Kamati ya mazingira kijijini hapo ndugu Sosteness Maseli na Enock Edward waliishukuru wilaya kwa kupanga kufanyika kwa sherehe hizo katani hapo kwani Elimu hiyo imewasaidia katika masuala ya kunawa mikono na matumizi bora ya choo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.