MAADHIMISHO YA WIKI YA UNYONYESHAJI YAFANA KARAGWE
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji wilayani hapa yamehitimishwa hivi karibuni katika kijiji cha Kanoni huku mada mbalimbali kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama zikitolewa kwa akina mama na wananchi wote waliokusanyika katika viwanja vya zahanati ya Kanoni.
Kupitia maadhimisho hayo, Afisa Lishe wa Wilaya, Selemani Khamis aliwasilisha mada kwa wananchi hao kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama ambapo aliwahimiza akina mama waliokukwa wamekusanyika kwa wingi katika eneo hilo juu ya swala la unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo pasipokumpa mtoto chakula chochote huku akibainisha ya kwamba maziwa ya mama ndicho kinapaswa kuwa chakula pekee cha mtoto kwa kipindi hicho.
“Faida za kunyonyesha maziwa ya mama pekee ni pamoja na kumpatia virutubisho vyote mtoto kwa uwiano sahihi kwa ukuaji na maendeleo yake, maziwa ya mama humpatia kinga mtoto dhidi ya maradhi mbalimbali ya kuharisha na magonjwa ya njia ya hewa, maziwa ya mama huyeyusha kwa urahisi na hufonzwa na mwili kwa ufanisi na kipekee huleta uhusiano mzuri na wa karibu kati ya mama na mtoto na maziwa ya mama hayana gharama”, alisisitiza Selemani katika utoaji wa mada.
Kwa upande mwingine, Selemani kupitia mada hiyo aliweza kugusia athali/madhara yanayoweza kumpata mtoto ambaye hakunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanza tangu kuzaliwa kwake ambapo baadhi ya athali zilibainishwa zilikuwa kama vile utapiamlo, kuhara mara kwa mara, magonjwa ya njia ya hewa na wakati mwingine kusababisha kifo.
“Ili mama aweze kumnyonyesha mtoto wake vizuri hadi kufikia miaka miwili inabidi mama afanye maandalizi wakati wa ujauzito kwa kupata lishe bora na kuendelea na lishe bora kipindi chote cha unyonyeshaji”, alisema Selemani.
Katika hatua nyingine Selemani alizitaja baadhi ya changamoto zinazochangia mama kutokumnyonyesha mtoto ipasavyo ambapo ilielezwa kwamba mama kutokumpa maziwa ya mwanzo ya njano mtoto pindi anapozaliwa, mama kuwa na kazi nyingi au kuwa mbali na mtoto, mlo wa mama anayenyonyesha, msongo wa mawazo, mama mwenye utapiamlo na imani zinazohusiana na mila na desturi zisizofaa kuwa ni baadhi ya changamoto zinazoathiri suala la unyonyeshaji.
Aidha, Selemani alifafanua ya kwamba maziwa ya mama ya mwanzo ambayo huwa na rangi ya njano hayapaswi kumwagwa kama ambavyo wengi wamekuwa wakifanya na kutoa wito kwa akina mama kuwanyonyesha watotowao maziwa hayo ambayo aliyataja kuwa yana kingamwili zinazoweza kusaidia kumlinda mtoto dhidi ya maradhi.
Wito mwingine ulitolewa kwa akina mama ilikuwa ni suala la kutokuwapa maji ya kunywa watoto walio chini ya umri wa miezi sita kwani maziwa ya mama yanatajwa kuwa kiwango cha kutosha cha maji na hii ni kutokana na ukweli wa kwamba watoto hawahitaji kiasi cha maji ya ziada.
Naye Mgeni Rasmi katika sherehe hizo, Diwani wa Kata ya Kanoni, Mh. Sabby Rwazo alisisitiza baadhi ya mambo yayofundishwa katika mada huku akitoa rai kwa akina mama kuzingatia agizo la kutokuwapa watoto walio chini ya umri wa miezi sita vyakula vya nyongeza tofauti na maziwa huku akisisitiza wananchi hao kuitilia mkazo kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2018 inayosema “Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama ni Msingi wa Maisha” huku akieleza ya kwamba kama wananchi hao wataendana na kauli mbiu hiyo ni dhahiri kuwa suala la udumavu ambao huathiri makuzi ya mtoto ya kimwili na ubongo vitabaki kuwa historia katika wilaya ya Karagwe.
Aidha Mh. Rwazo, aliweza kutoa wito kwa wanaume kuwapunguzia kazi wake zao ili waweze kupata muda wa kunyonyesha watoto huku akitaja ushiriki wao huo kuwa ni muhimu sana katika suala la kuboresha afya na lishe ya familia.
Katika hatua nyingine Mgeni Rasmi aliweza kutoa zawadi kwa mama aliyefanikiwa kumleta mtoto wake kliniki bila kukosa ambapo zawadi hiyo ilitolewa kwa mama mmoja aliyejulikana kwa jina la “Mama Brayan
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.