DC LAIZER ASISITIZA ELIMU ZAIDI ITOLEWE KWA WANANCHI JUU YA BIMA YA AFYA KWA WOTE.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mhe. Julius Kalanga Laizer, amewaagiza watendaji wote wa Serikali kuhakikisha wanatoa Elimu zaidi kwa jamii ili suala la bima ya afya kwa wote liwafikie wananchi.

Ameyasema hayo Januari 06, 2026 wakati akifungua kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri (Angaza).
Mhe. Laizer ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuzindua mpango wa bima ya afya kwa wote mwezi Januari.
“Bima ya afya kwa wote iwe agenda ya kudumu katika vikao vyote vitakavyofanyika kuanzia ngazi ya kijiji, Kata na vikao vyetu vya utendaji kwa sababu ni moja ya ahadi ambazo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi kutimiza ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”
“Ili kuunga mkono juhudi za Serikali, tunatakiwa kuhakikisha elimu juu ya umuhimu wa bima ya afya kwa wote inawafikia wananchi kwa ukaribu,” aliongeza Mhe. Laizer.

Kwa upande wake, Mratibu wa Bima ya Afya Wilaya ya Karagwe Ndg; Desderius Tumaini Buhiye ameeleza kuwa bima ya afya kwa wote itatolewa kwa kaya ikihusisha baba, mama na watoto wanne.
“Serikali imedhamiria kuhakikisha Watanzania wanapata matibabu bila kuumizwa, ndiyo maana imeanzisha bima ya afya kwa wote itakayogharimu shilingi laki moja na nusu (150,000/=) kwa mwaka mzima na bima ya afya itatoa nafasi kwa kaya maskini, Wazee na watu wenye ulemavu. Alisema Ndg; Buhiye

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe Bi; Happiness Msanga, aliahidi kuendelea kufanya ufuatiliaji ili kuhakikisha elimu juu ya bima ya afya kwa Wote inatolewa na kuwafikia wananchi.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bi; Agness Mwaifuge alieleza juu ya Bima ya Afya kwa Wote kuwa itatolewa kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospital ya Wilaya kwa huduma za dawa na vifaa tiba 247, Huduma za upasuaji mdogo 27 na Huduma za upasuaji Mkubwa 9 kwa gharama hizo hizo za Bima.

KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.