COSTECH yadhamiria Mapinduzi ya Viwanda.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Chuo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku kilichopo wilayani Bukoba, Mkoani Kagera kwa pamoja wamedhamiria kwa dhati kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. Dkt John Pombe Joseph Magufuli za kuifanya Tanzania ya viwanda kupitia sekta ya kilimo.
Jitihada hizo katika kufikia mapinduzi hayo ya kilimo zinajidhihirisha kupitia mradi unaotekelezwa kwa pamoja baina ya taasisi hizi mbili wa kusambaza mbegu bora za mihogo zijulikanazo kwa jina la “Mkombozi” zenye uwezo pia wa kupambana na ugonjwa maarufu unaoshambulia na kuathiri mazao ya mihogo mkoani Kagera ujulikanao kwa jina la Batobato.
Mnamo tarehe 25 Oktoba, 2017 wataalam kutoka taasisi hizo walifika wilayani hapa kwa lengo ya kusambaza mbegu pingili 8,000 zinazotajwa kwamba zitaongeza thamani ya uzalishaji wilayani hapa.
Mara baada ya wataalam hawa kuwasili wilayani hapa waliongozana na viongozi wa wilaya hii kwenda kwenye vijiji viwili vilivyochaguliwa kuwa mashamba darasa katika uzalishaji wa mbegu hizi za mihogo wilayani Karagwe.
Msafara huo uliokuwa umeambatana na Mkuu wa Wilaya Karagwe Mh. Godfrey Mheluka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mh. Wallace Mashanda, Diwani wa Kata ya Nyakahanga Mh. Charles Beichumila, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ndugu Ashura Kajuna pamoja na baadhi ya wataalam kutoka katika Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika ulianza kazi hiyo katika kijiji cha Bisheshe Kata ya Nyakahanga.
Mara baada ya kufika katika kijiji hicho msafara huo ulianza kufanya kazi ya kusambaza mbegu za mihogo ikiwa ni pamoja na kuonesha kwa vitendo jinsi mbegu hizo zinavyopambwa.
Kabla ya onesho hilo la upandaji wa mbegu hizo, Dkt. Beatrice Lyimo na ndugu Bestina Daniel ambao ni watafiti toka COSTECH walisisitiza mambo kadhaa ikiwemo kuzingatia kanuni na taratibu za kilimo ili kuvifanya vijiji hizi zilivyochaguliwa kama mashamba darasa kwa ajili ya kuzalisha mbegu hizi kwa ufanisi ili baada ya vijiji hivi vya Nyarugando kilichopo katika Kata ya Rugera na Bisheshe kilichopo katika kata ya Nyakahanga viweze kuwasaidia wakulima wengine katika kata zote wilayani hapa katika kupata mbegu hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh.Godfrey Mheluka aliwashukuru sana COSTECH kwa namna walivyobuni wazo hilo ambapo alitaja kuwa ni mkombozi katika shughuli za kilimo wilayani hapa.
“Napenda kuwashukuru COSTECH kwa jambo hili lakini nikushukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe kwa maandalizi haya, wito wangu kwa wataalam wa Kilimo ni kuwasimamia wataalam wa kilimo wilayani hapa ili waweze kuyafanya mashamba haya kuwa sehemu muhimu ya usamabazaji wa mbegu wilayani hapa” alisema Mh. Mheluka kwenye kijiji cha Bisheshe.
Mheluka aliongeza na kusisitiza,” Nitafuatilia kwa nguvu zangu zote kuona kinachoendelea hapa Bisheshe na kwa kweli nisingependa kuona uzembe katika usimamizi wa mradi huu”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Mashanda aliwasihi wananchi wilayani hapa kuchangamkia fursa hii ya kilimo cha zao la muhugo.
“Serikali ina mpango wa kujenga kiwanda cha mihogo wilayani Biharamulo kwa hiyo niwatoe hofu wananchi kwamba suala la soko la zao hili halitakuwa changamoto tena kutokana na kujengwa kwa kiwanda hicho kitakachokuwa kinahitaji malighafi ya zao la hili kwa wingi”, alisema Mh. Mashanda.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ndugu Ashura Kajuna alitumia wasaa huo kuwashukuru wadau hao wa maendeleo huku akiwahakikishia kwamba jitihada zao hazitapotea bure kwani ofisi yake itasimamia kikamilifu ili kuhakikishia vijiji hizi vya Bisheshe na Nyarugando vinakuwa mfano kwa maeneo mengine yanayotarajiwa kugawiwa mbegu hizi za mihogo hapo baadae.
Baada ya maelezo hayo, Mtaalam kutoka Chuo cha kilimo cha Maruku ndugu Georgina Kibura ambaye ndiye aliyekuwa na jukumu muhimu la kuonesha jinsi mbegu hizi zinavyopandwa aliwaongoza washiriki kwenda kwenye shamba hilo lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya kupandwa mbegu hizo.
Mtaalamu huyu alitoa maelekezo kwa wakulima kikundi cha wakulima kwamba upandaji wa mbegu hizi unatakiwa kuwa ni mita 100 kati ya mstari na mstari na kati ya mche na mche inapaswa kuwa mita moja.
“Kuna faida za kuzingatia vipimo hizi katika kilimo ikiwemo kusaidia kurahisisha shughuli mbalimbali za kilimo kama vile palizi na hata shughuli za uvunaji,” alisema ndugu Georgina.
Huku akiwashauri kutopanda mazao mseto kwenye shamba hilo darasa, ndugu Georgina aliwaambia wakulima kutokufanya hivyo ili kuwe na taswira nzuri ya inayoakisi shamba darasa la mihogo.
Aliendelea kusisitiza kwamba wakati wa upandaji wa miche hiyo wakulima watapaswa kuzingatia kwamba wanaacha mafundo mawili juu.
Huku akisisitiza kwamba kama wakulima hao watazingatia maelekezo hayo aliyowapa na maafisa ugani wakafanya jitihada kubwa za kuwasimamia wakulima hao basi kuna uwezekano mkubwa wa kuzalisha kiasi cha tani 32 kwa hekari moja waliyopanda.
Baada ya kumaliza kazi hiyo kwenye kijiji cha Bisheshe, msafara huo uliendelea katika kijiji cha Nyarugando ambapo hata hivyo shughuli hiyo haikufanyika kutokana na ushauri uliotolewa na Dkt. Beatrice Lyimo kutokana na mazingira ya kijiji hicho kutokupata mvua hivi karibuni ambapo kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na wataalamu ilionekana kwamba ni vyema wanakikundi hawa wa Chamanya Saccos wakaendelea na shughuli nyingine za maandalizi na kuahidi kuwa wakati wowote mvua zitakaponyesha wataweza kuwaletea mbegu hizo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halamshauri ya Wilaya na Diwani wa Kata hiyo ya Rugera Mh. Dawson Paulo Byamanyirwohi aliyekuwapo katika eneo hilo kwa kuona umuhimu wa ushauri huo uliotolewa alikubaliana na wataalam hao huku akiwaomba wananchi hao kuwa na subira kwani wataalam hao watawaletea mbegu hizi kama walivyoahidi huku akimwagiza Mkuu wa Idara ya Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji ndugu Adam Salum wa Wilaya kuhakikisha wanaifanyia kazi changamoto ya kutokupata mafunzo walioitoa wanakikundi cha Chamanya Saccos kupitia risala yao ya kwamba licha ya mafanikio ya kuunda ushirika huo lakini wanayo changamoto ya kukosa mafunzo hayo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.