Chuo Kikuu cha Karagwe kuzinduliwa Oktoba 29, 2017
Na Geofrey A. Kazaula - Karagwe
Chuo kikuu cha Karagwe ( KARUCO) kinacho milikiwa na Kanisa la kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Karagwe kina tarajiwa kuzinduliwa rasmi mnamo tarehe 29/10/2017 ambapo wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi watashiriki uzinduzi huo wakiwemo viongozi wa ngazi za juu wa Kitaifa.
Waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe pamoja na viongozi wa chama cha Mapinduzi wamefanya ziara katika chuo hicho baada ya kupokea mwaliko wa Askofu Benson Bagonza ili kufanya ukaguzi wa miundombinu na kujenga uelewa wa pamoja kabla ya uzinduzi rasmi wa chuo kufanyika.
Ziara hiyo pia imehusisha wataalam mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya ya Karagwe ambapo wameweza kutembelea sehemu mbalimbali za chuo hicho na kujionea mundombinu iliyo kamilika na inayoendelea kujengwa.
Hadi sasa tayari miundombinu ya maji imekamilika kwa sehemu kubwa, Bweni la kulala wanafunzi wa kike limekamilika, jengo la utawala limekamilika, maabara zote zinazohitajika zimekamilika pamoja na Maktaba .
Miundo mbinu nyingine pia imekamilika ikiwemo madarasa na samani mbalimbali zitakazotumiwa na wanafunzi zimewekwa.
Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, Miundombinu mingi imechangiwa na wanachi wa Karagwe pamoja na waumini na pia wahisani nao wamechangia na wanaendelea kuchangia ili kuhakikisha Karagwe inakuwa na chuo kikuu cha mfano.
Akifafanua juu ya Kozi zitakazo anza kutolewa na chuo hicho Askofu Bagonza amesema kuwa wataanza na kozi nne ambazo ni Kilimo, Mifugo, Misitu na Mazingira na kwamba kozi nyingine zitafuatia badae.
Aidha, amezitaja baadhi ya fursa ambazo wananchi wa Karagwe watanufaika nazo ikiwemo kupanua soko la mazao yao na mifugo na kuikuza Wilaya kiuchumi baada ya kuwa na wataalam karibu ambao pia watasaidia katikakuongeza thamani katika mazao ya wakulima na kutafuta soko. la pamoja.
Kwaupande wao waheshimiwa madiwani wamepongeza jitihada zilizofanywa na Kanisa na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutoshaili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Kuhusu migogoro ya ardhi iliyojitokeza siku za nyuma, waheshimiwa madiwani wamefafanua kuwa migogoro hiyo ilikuwa inachochewa na watu wa chache wasiopenda maendeleo na kwamba tayari migogoro imekwisha na sasa ni kufanya maendeleo kwaajili ya watu wa Karagwe na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Askofu Bagonza ame eleza kufurahishwa na ushirikiano anaopata kutoka kwa viongozi wa wilaya tangu miaka ya 1980 hadi sasa ambapo wanaenda kushuhudia hatua kubwa sana ya maendeleo Karagwe.
Wah, madiwani wamemtaka Askofu huyo kuwapuuza watu watakao taka kurudisha nyuma jitihada zinazoendelea kufanyika kwaajili ya maendeleo na kwamba Serikali haitakuwa tayari kuvumilia watu wanaotaka kukwamisha maendeleo ya wananchi.
Kuhusu umiliki wa chuo, imefafanuliwa kuwa chuo hicho ni mali ya wananchi wa Karagwe bila kujali tofauti zao za kiimani na kwamba kinaendelea kuchangiwa na watu mbalimbali kwani kinalenga kwenye mapinduzi ya kiuchumi na kijamii Wilayani Karagwe.
‘’Licha ya chuo hiki kusajiliwa kwa jina la Kanisa lakini ni mali ya wananchi wote wa Karagwe na kinaendelea kuchangiwana waumini wa dini zote hivyo natoa wito kwa kila mmoja wetu kuunga mkono jitihada hizi ili kuinua maendeleo ya wilaya yetu na taifa kwa ujumla.’’ alisema Askofu Bagonza
Ili kuwezesha wakulima kupata soko nzuri la mazao yao, Askofu Dkt Bagonza amebainisha kuwa mara baada ya chuo kuzinduliwa, upo mpango wa kujenga vituo vya fursa vitano( Opportunity Centers ) ambapo vituo hivyo vitakuwa na miundombinu ya kila aina ikiwemo ya kuhifadhi mazao yasiharibike na kwamba wakulima watakuwa wanauzia mazo yao katika vituo hivyo kwa umoja ili wawe na sauti ya pamoja ya kupanga bei ya mazao tofauti na ilivyo hivi sasa
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.