Bashungwa Amwangukia Rais Magufuli Mradi wa Maji Ziwa Rwakajunju
Na Geofrey A. Kazaula – KARAGWE.
Mbunge wa jimbo la Karagwe, Mh. Innocent L. Bashungwa amemwomba Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mh, John Pombe Magufuli kusaidia katika kukamilisha mradi wa maji wa Rwakajunju ili kuwatua ndoo kichwani wananchi wa Karagwe hususani akina mama.
Maombi hayo kwa Rais yametumwa kupitia aliyekuwa mgeni Rasmi katika uzinduzi wa majengo na miundombinu ya kinachotarajiwa kuwa chuo kikuu cha Karagwe ( KARUCO) Mh, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ambaye naye pia aliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mh, Meja Jenerali ( Mst) Mustafa S.Kijuu baada ya Mh, Kikwete kushindwa kufika kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezowake.
“Mradi huu wa maji ulianza kupangwa tangu kipindi cha awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete lakini hadi sasa haujawahi kukamilika, Mh Rais Mstaafu, nakuomba ufikishe kilio hiki kwa Rais Magufuli ili mradi huu uweze kuanza kwani shida ya maji kwa Karagwe nikubwa mno, naongea hivi nikiwa nimepiga magoti kama ishara ya kuonesha ukubwa wa tatizo hili”, alisema Mh. Bashungwa.
Kwa vipindi tofauti, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha huduma za kijamii zinapatikana na kuwafikia wananchi kwa urahisi, ufanisi na kukidhi mahitaji.
Pamoja na jitihada hizo , huduma ya maji kwa mji wa Kayanga na baadhi ya vijiji Wilayani Karagwe imekuwa ya kiwango cha kutoridhisha kutokana na halihalisi ya jiografia ya eneo lenyewe kwani vyanzo vya maji vilivyopo katika baadhi ya maeneo havina maji ya kutosha .
Licha ya vyanzo vingi vya maji kutokuwa na maji ya kutosha, vyanzo hivyo vinapatikana katika maeneo ya mabondeni huku makazi ya watu yakiwa maeneo ya juu kwenye miinuko na hivyo kuhitaji gharama kubwa za ujenzi wa miradi ya maji na uendeshaji wake.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ilishaweka katika mipango yake Mpango wa usanifu na hatimaye ujenzi wa mradi wa maji kwa manufaa ya wakazi wa makao makuu ya mji wa Wilaya na vijiji vyote jirani .
Hata hivyo, kuna vijiji 30 vilivyopendekezwa kunufaika na mradi huu wa maji kutoka ziwa Rwakajunju ambapo vijiji hiyo ni Ahakishaka, Kashanda , Ndama, Nyabiyonza, Nyamieri, Nyabwegira, Chabalisa , Nyakagoyagoye, Kagutu, Kafuro, RularoKishoju na Nyakaiga.
Vijiji vingine ni Kiruruma, eneo linalotajiwa kuwa chuo Kikuu cha Karagwe – KARUCO University, Kakuraijo, Kamagambo, Mlamba, Omukakoto, Chonyonyo, Nyamizi, Nyakashenyi, Omukimeya, Katembe, Nyakisheshe, Ihanda, Bisheshe Omurusimbi, Rukole na Kituntu.
Hadi sasa kazi inayotarajiwa kukamilika ni kukamilisha upembuzi yakinifu na kuingiza vijiji vyote kwenye mwambao wa mradi.
Kwa mujibu wa ‘BUWASA’ ambao wanasimamia zoezi hili kwa niaba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji wamesema kwamba wanatarajia kuwa taratibu za kumpata mshauri elekezi utakuwa umekemilika mapema mwishoni mwa mwezi Januari 2018 .
Miongoni mwa kazi za mshauri elekezi itakuwa ni pamoja na kukamilisha ‘design’ na kuandaa makabrasha ya zabuni .
Mradi wa maji kutoka ziwa Rwakajunju unakadiriwa kugharimu dola za kimarekeni millioni 70.7 ambapo kilio cha mbunge wa jimbo la Karagwe ni kuona serikali inatoa fedha hizo kwa wakati ili mradi uanze kwani changamoto ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Karagwe nikubwa sana.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.