BARAZA LA MADIWANI LAWEKA MIKAKATI NA MAAZIMIO KADHAA KWA AJILI YA SHUGHULI ZA MAENDELEO
Na Innocent E. Mwalo.
Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Agosti 01- 02, 2018 katika Ukumbi wa Kituo cha Vijana Rafiki cha Angaza kimemalizika kwa kuweka maazimio kadhaa wa kadhaa yenye lengo la kuongeza wigo wa kukusanya mapato na kuboresha wigo wa kuwahudumia wananchi.
Katika kikao hicho cha robo ya nne kwa mwaka wa Fedha 2017/2018, wajumbe walijadili taarifa mbalimbali na kuweka maazimio katika maeneo kadhaa kwa ajili ya kuiwezesha Menejimenti kufanya ufuatiliaji wa kina kwenye maeneo hayo lengo likiwa ni kuongeza tija katika utoaji wa huduma.
Baadhi ya maazimio yaliyowekwa na kikao hicho yalikuwa ni katika suala la usafi wa mazingira ambapo katika Halmashauri hii, ratiba yake huwa ni siku ya Alhamisi kila wiki na Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi.
Baada ya mjadala uliochukua muda mrefu katika eneo hili, Baraza liliazimia kwa kauli moja jambo hili kusimamiwa kikamilifu ili hali ya usafi iliyotajwa kuzorota irejee katika hali yake ya kuridhisha.
Azimio jingine ambalo liliwekwa lilikuwa likienda sambamba na agizo kwa Idara ya Afya kuziagiza Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati kufuatilia kote wilayani hapa ili kuhakikisha kwamba wananchi hawakosi dawa katika maeneo hayo kutokana na tatizo lililolipotiwa na wajumbe wengi wa kikao hicho la kukosekana kwa dawa kwenye baadhi ya maeneo hayo ya kutolea tiba wakati fedha zipo kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.
“Aidha tunapenda kuazimia kuwa Menejimenti ivisimamie na kuvisaidia vijiji vyote ili kwa msaada wa Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya viweze kutengeneza sheria ndogo zitakazosaidia katika ukusanyaji wa mapato”, alisikika Mh. Wallace Mashanda, Mwenyekiti wa Halmasahuri ya Wilaya.
Kupitia kikao hicho, Baraza liliazimia wananchi Wilayani hapa kupewa Elimu kuhusu gugu karoti, mmeo unaotajwa na wataalamu wa sekta ya kilimo kwamba umeleta madhara makubwa kwa wanyama na mimea huku wito ukitolewa kwa wananchi kufyeka gugu hilo kwenye maeneo yao na kulichoma moto lakini pasipo kusababisha athali za uchomaji wa moto ovyo.
Azimio jingine lililowekwa ilikuwa ni juu ya utelezaji wa sheria inayohusu mifugo kusafirishwa barabarani huku wito ukitolewa kwa wananchi kufuata taratibu kwa mujibu wa sheria katika kusafirisha mifugo kutoka eneo moja kwenda eneo jingine huku ikitajwa kufanya hivyo kuwa kinyume cha sheria za nchi na kwa yeyote anayekiuka kupaswa kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yake.
Agizo jingine lilikuwa ni kwa watumishi wote wenye vitabu vya kukusanyia mapato ambavyo kimsingi vilipaswa kuwa vimerejeshwa kwenye ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kupitia kwa Mweka Hazina wa Wilaya, na katika eneo hili iliagizwa kwa msisitizo mkubwa kwa wote wenye vitabu hivyo kuvirejesha ndani ya siku 14 huku ikiazimiwa hatua kali zichukuliwe kwa mujibu wa sheria wote watakaokiuka agizo hili.
Azimio jingine ilikuwa ni kwamba katika kila kikao cha robo Baraza lipokee na kujadili taarifa za mimba mashuleni pamoja na kueleza vifo vya akina mama na watoto vinavyokuwa vimetokea kwa wakati husika.
Katika hatua nyingine, Baraza lilipokea taarifa ya Serikali iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka ambapo baadhi ya maelekezo katika taarifa hiyo ilikuwa ni agizo kwa wananchi wote wilayani hapa kuwafichua watu wote wanaojihusisha na wizi wa mifugo na utekaji wa watoto vitendo ambavyo hapo awali vilitajwa na wajumbe wa kikao hicho kwamba vimekithiri katika Wilaya hii.
“Kupitia kikao hiki napenda kuwaagiza wananchi wa Wilaya za Karagwe, Kyerwa na Missenyi kuepuka kuuza kahawa kwa njia ya magendo, kuuza kahawa mbichi na kuuza kahawa kwa njia ya ‘butura’ na niwahakikishie ya kwamba serikali ipo kazini kwenye maeneo hayo na kamwe hatutamvumilia mtu yeyote atakayekwenda kinyume na maagizo ya serikali ambapo imeagizwa kahawa yote iuzwe kupitia vyama vya ushirika”, alisema Mh. Mheluka.
Aidha katika hatua nyingine Mh. Mheluka alitumia kikao hicho kuutangazia umma juu ya kuundwa kwa Baraza la Wafanyabiashara wilayani hapa ambalo alilitaja kuwa litakuwa na wajumbe takribani 40 lengo likiwa ni kuchochea shughuli za biashara na kuhimiza wananchi juu ya ulipaji wa kodi.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.