Baraza la Madiwani Latoa Maagizo kwa Wananchi, Watendaji.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Kikao cha Baraza la Madiwani kilichodumu kwa takribani siku mbili kimemalizika Novemba 30, 2017 huku wajumbe wa Baraza hilo wakiweka mipango na mikakati kadhaa katika kuboresha suala la ukusanyaji wa mapato, utoaji bora wa huduma za Elimu, Afya na Maji huku pia masuala ya kilimo, ujenzi wa miundombinu na uhifadhi wa mazingira yakipewa msisitizo mkubwa kupitia kikao hicho.
Aidha katika kikao hicho ajenda ya kudhibiti UKIMWI wilayani hapa ilipewa kipaumbele.
Katika kuboresha ukusanyaji wa mapato wilayani hapa wajumbe wa Baraza la Madiwani kwa kauli moja waliunga mkono suala la kufungwa kwa mnyororo katika stendi ya Kishao kwa ajili ya kuongeza ukusanyaji wa ushuru wa teksi ambapo wajumbe wengi waliagiza jambo hilo kukamilika kwa wakati.
Katika kuonesha kwamba suala la ukusanyaji wa mapato linakuwa na msisitizo wa aina yake, wajumbe wa Baraza la Madiwani walimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hii ndugu Godwin Kitonka kuhakikisha anaitisha kikao cha Watendaji wa Kata ili waweze kupata semina Elekezi juu ya masuala ya ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yao pamoja na kupewa mwongozo juu ya waraka unaonesha ni kitu gani wanapaswa kukusanya na kipi hawapaswi kukusanya ili kuondoa mkanganyiko uliopo hivi sasa baina ya watendaji juu ya jambo hilo.
Aidha katika kikao hicho, Baraza liliagiza kwamba kila mtendaji wa Kata anapaswa kuwa na mpango mkakati wa malengo ya kukusanya mapato kwenye eneo lake kwa kila mwezi na iliagizwa kwamba kila mmoja apimwe ufanisi wake katika malengo aliyofikia juu ya jambo hilo.
Kuhusu sekta ya Elimu ushauri ulitolewa na wajumbe wa kikao hicho kwa wakuu wa Idara za Elimu Msingi na Sekondari kuuona ufaulu wa shule Mt. Peter Clavery iliyopo kwenye kata ya Bugene ambayo kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania, NECTA shule hiyo imekuwa ya kwanza kitaifa kwa matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2017.
“Kwa kweli suala la shule ya Mt. Peter Clavery katika matokeo ya darasa la saba limetutoa kimasomaso wananchi wa Wilaya ya Karagwe na mkoa wa Kagera kwa ujumla na hii iwe ni changamoto kwa maafisa Elimu wetu kuiona hiyo kama changamoto kwa shule zetu za serikali ili ziweze kufanya vizuri kama zinavyofanya shule hizo za binafsi”, alisisitiza Mh. Novati Kishenyi Diwani wa Kata ya Chonyonyo.
Kuhusu sekta ya Afya kikao hicho kilipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na wadau wa maendeleo wa shirika la maendeleo la Rugu ADP hasa katika ujenzi wa zahanati na shule wilaya hapa na wajumbe kwa kauli moja walikubaliana kutolewa kwa cheti cha pongezi kwa wadau hao wa maendeleo ili kutambua kuenzi mchango wao.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Wakala wa Barabara, Mjini na Vijijini, Mhandisi Peter Mikimba aliweza kuwasilisha taarifa inayohusu ujenzi wa barabara wilaya hapa kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo alitaja mtandao wa barabara tano zinazotarajiwa kujengwa kwa kipindi hicho ambazo zinatajwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 700.
Aidha katika kikao hicho lilitolewa agizo kwa maafisa Elimu wilayani hapa kutoa maagizo kwa walimu wakuu na wakuu wa shule juu ya suala la kukomeshwa kwa biashara ya chuma chakavu mashuleni kufuatia wito uliotolewa na Diwani wa Kata ya Kiruruma, Mh Evarista Sylivester kwamba kuna suala limeibuka la wafanyabiashara kuwatumia watoto wa shule katika kufanya biashara ya chuma chakavu.
“Hatutaki yatukute madhara yaliyotokea wilayani Ngara hivi karibuni kwa watoto kulipukiwa na bomu lilidhaniwa kama chuma lilipookotwa na watoto hivi karibuni”, alisikika Mh. Wallace Mashanda.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.