Baraza la Madiwani Lapitisha Bajeti ya Tsh 52,557,611,988.94 kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya hii limehitimisha kikao chake maalum cha Bajeti mnamo Januari 30, 2018 kwa kupitisha Bajeti ya kiasi cha jumla Tsh. 52,557,611,988.94 kwa ajili ya shughuli za maendeleo Wilayani hapa.
Uamuzi wa kupitisha kiasi hicho cha Fedha ulitangazwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe Mh. Wallace Mashanda baada ya kuwahoji wajumbe wa kikao hicho ambao ni waheshimiwa madiwani ambapo kwa zaidi ya asilimia 98 waliafiki kupita kwa kiasi hicho cha Bajeti.
Kupitishwa kwa kiasi hiki cha Bajeti kunafanya ongezeko la Bajeti kwa kiasi cha Tsh. 5,540,209,962.38 ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo jumla ya Tsh.47,017,402,026.56.
Kabla ya kupitishwa kwa Bajeti hiyo wajumbe wa kikao hicho walijadili kwa kina na kuboresha maeneo kadhaa ya utekelezaji wa Bajeti hiyo na kisha waliafiki Bajeti hiyo inayohusisha Makisio ya Mapato ya ndani yakiwa ni kiasi cha TZS. 1,958,547,520.00, Asilimia 40% ya Mapato ya ndani (Miradi ya maendeleo) yenye jumla ya kiasi cha Tsh. 783, 419,008.00, Asilimia 60% ya Mapato ya ndani (Matumizi ya Kawaida) ikiwa ni kiasi cha Tsh.1,175,128,512.00.
Vyanzo vingine vya mapato kwa mujibu wa kikao hicho ni Ruzuku ya Matumizi Mengineyo/Kawaida kiasi cha Tsh. 1,473,381,361.04, Ruzuku ya Mishahara (PE) kiasi cha Tsh.38,924,366,436.00, Miradi ya Maendeleo ikiwa na kiasi cha Tsh.9,919,740,679.90
Aidha vyanzo vingine vilihusisha Mchango wa wananchi wenye jumla ya kiasi cha Tsh. 765,000,000.00 pamoja Mchango wa taasisi zisizo kuwa za kiserikali (NGOs) zinazotajiwa kuchangia kiasi cha Tsh. 300,000,000.00 katika Bajeti hii.
Pamoja na kutengwa kwa Bajeti hii wajumbe walichangia kwa angalizo na msisitizo mkubwa juu ya kuiomba serikali kuu kuleta Fedha za Miradi kwa wakati kwani katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2017/2018 Halmashauri iliidhinishiwa kutumia jumla ya Tsh.47,017,402,026.56 ili kutekeleza Miradi ya Maendeleo, Mishahara ya watumishi, Matumizi mengineyo na mapato kutokana na vyanzo vya ndani lakini hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2017, Halmashauri ilikuwa imepokea jumla ya TZS. 14,698,093,583.82 sawa na asilimia 31.26 tu ya bajeti nzima ya Halmashauri.
Kwa upande wa matumizi iliripotiwa kwamba hadi kufikia tarehe 31/12/2017, Halmashauri ilikuwa imetumia jumla ya Sh. 14,487,059,929.59 sawa na asilimia 98.56 ya Mapato yote.
Kwa upande wa vipaumbele katika Bajeti hii ni ununuzi wa gari moja kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa magari.
Vipaumbe vingine vya mpango wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha huu vinahusisha kuendeleza sekta ya kilimo hasa mnyororo wa thamani kwa zao la kahawa ambapo Halmashauri imeshauriwa kutengwa hadi kiasi cha sh. 80,000,000 kwa ajili ya kuboreshwa kwa zao hili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kipaumbele kingine ni ujenzi wa soko la Kayanga baada ya kuungua moto mara mbili mnamo mwaka 2016 ambapo ili kufikia kipaumbele hiki Halmashauri imetenga kiasi cha Tsh.190,000,000 kwa ajili ya kuanza shughuli hiyo.
Halmashauri imetenga pia kiasi cha Tsh.80,000,000 kwa ajili ya kusaidia kukuza na kuendeleza viwanda vidogo vidogo wilayani hapa.
Hali kadhalika Halmashauri imetenga kiasi cha Tsh.90,000,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi ya mabasi Kishao.
Kipaumbele kingine ni kuendeleza na kukuza uchumi wa makundi mbali ya wanawake na vijana kwa kutenga jumla ya Sh. 182,487,552 kwa shughuli hiyo.
Pia, Halmashauri imeendelea kutenga Fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi, wazabuni mbalimbali na watumishi ambapo kiasi cha Tsh.235,092,111.90 kimetengwa kwa shughuli hiyo.
Vipaumbele vingine ni pamoja na Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi kuendelea kukamilisha maabara za Sayansi katika Shule 19 za sekondari za serikali ambapo kiasi cha Tsh.200,000,000 zimetengwa kwa shughuli hiyo.
Kikao hicho pia kilikubaliana kuimarisha mifumo mbalimbali ya kukusanyia mapato na ile ya kibajeti kuimarishwa ambapo mkazo uliwekwa kuimarisha mfumo kibajeti yaani PlanRep, mfumo wa kiutumishi(HCMIS), mifumo ya kutolea taarifa yaani CDR na CFR pamoja na ile ya kiuhasibu ya IPSAS na EPICOR ambapo kiasi cha 19,960,000 kimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
Kujengwa kwa Hospitali ya Wilaya ni kipaumbele kingine ambapo jumla ya Tsh.100,000,000 kimetengwa ili kuruhusu kuanza kwa shughuli hiyo.
Bajeti hii inatarajiwa kujadiliwa na kupitishwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye kikao chake cha Bajeti kinachotarajiwa kuketi mapema kuanzia mwezi Aprili mwaka huu mjini Dodoma. Vikao vingine vinavyotajiwa kujadili mapendekezo ya Mpango huu wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 ni kile cha ushauri cha mkoa (RCC) kinachotarajiwa kukutana mjini Bukoba mnamo Februari Mosi, 2018.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.