Baraza la Madiwani lapiga “stop” kwa muda shughuli za uvuvi
Na Innocent Mwalo, KARAGWE.
Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Wilaya Karagwe kupitia kikao chake cha robo ya pili kilichofanyika hivi karibuni limepiga marufuku kwa muda shughuli zote za uvuvi.
Madiwani hawa kwa kauli moja waliazimia kusitishwa kwa muda shughuli za uvuvi kwenye maziwa yote yaliyopo katika wilaya hii ili kutekeleza kwa vitendo sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake zilizotolewa mwaka 2009 ambapo kwa pamoja zinaagiza kufungwa kwa shughuli zote za uvuvi kwa takribani miezi sita ili kuruhusu samaki kuzaliana na kukua.
“Waheshimiwa madiwani hii ni sheria na kweli tunapaswa kuisimamia na kwa mantiki hiyo nawaomba wataalam wetu na vyombo vya ulinzi na usalama wilayani hapa kusimamia kikamilifu usitishawaji wa shughuli za uvuvi kwa muda wa miezi sita yaani kuanzia tarehe 01/01/2018 hadi 30/06/2018 kwenye maziwa yote wilayani hapa”, alisisitiza Wallace Mashanda, mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya kupitia kikao hicho.
Azimio hili lililoungwa mkono kwa takribani asilimia mia moja na wajumbe wa Baraza la Madiwani akiwemo mbunge wa Karagwe, Mh. Innocent Bashungwa limepongezwa na baadhi ya wananchi walliohudhuria baraza hilo huku wengi wakisema uamuzi huo licha ya kwamba unaweza kuwa na maumivu kwa kipindi hiki lakini una tija hapo baadae kwani lengo lako ni kahakikisha kiwango cha samaki kinaongezeka na kukua na hivyo mara shughuli hizo zitakapoanza wananchi watapata fursa ya kufanya uvuvi wenye tija kwa kupata samaki wengi lakini pia wakubwa.
Kikao hicho kilichokuwa maalum kwa ajili ya kujadili taarifa mbalimbali kuhusu utendaji na uwajibikaji wa Halmashauri ikiwemo kupokea kwa taarifa za kamati za kudumu za Halmashauri ya wilaya pamoja na zile za Mkurugenzi Mtendaji.
Kwa upande mwingine kikao hicho kiliweza kufanya maboresho na mapitio kwa Bajeti ya Miradi ya maendeleo kwa mwaka 2017/2018 na ile ya mwaka 2018/2019 ili kutekeleza maagizo ya serikali kwa Halmashauri za Wilaya ya kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa na kumamilika kwa kipindi cha mwaka mmoja kama yalivyotolewa hivi karibuni.
Katika hatua nyingine kikao hicho kililaani vikali tukio la mwananchi mmoja ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mramba kata ya Kihanga kuvamiwa na watu wenye silaha na kumfanyia kitendo cha ukatili na kutoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama wilayani hapa kukomesha mara moja vitendo hivyo ambavyo vinalitia doa taifa hili na zaidi kupelekea viashiria vya uvunjifu wa amani.
Naye Mkuu wa Polisi wilayani hapa, Afande Mika Makanja alipokea agizo hilo na kuwaahidi wananchi wa Karagwe kupitia mkutano huo kwamba kamati yake ya uchunguzi ya jeshi la polisi inafuatilia kwa makini tukio hilo na kuahidi kuchukua hatua kali za kisheria kwa wahusika wote ili iwe fundisho kwa watu wengine.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.