Baraza la Madiwani Kujadili Bajeti ya Halmashauri Kifungu kwa Kifungu.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe limeanza kikao chake maalum kwa ajili ya kujadili na kupitisha Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 leo Jumatatu katika ukumbi wa Kituo cha Vijana Rafiki cha Angaza.
Kikao hicho kinachotajiwa kudumu kwa takribani siku mbili yaani tarehe 29- 30 Januari, 2018 pamoja na mambo mengine kwa tarehe 29/01/2018 kinatajiwa kupokea na kujadili Muhtasari wa Mapitio ya Bajeti ya Mwaka 2017/2018 na mapendekezo ya Bajeti kwa mwaka 2018/2019.
Aidha katika siku hiyo ya kwanza kikao hiki kitakuwa mahususi kwa ajili ya Majadiliano ya taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya juu ya Mapitio ya mpango wa 2017/2018 na mapendekezo ya Bajeti kwa Mwaka 2018/2019.
Mambo mengine yatakayopewa msukumo katika kikao cha siku ya kwanza ni pamoja kujadili mapitio ya mpango wa Bajeti kwa mwaka 2017/2018 pamoja na kupitia maoni na ushauri uliotolewa kwenye Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango na kikao cha Ushauri cha Wilaya yaani DCC.
Katika siku ya pili yaani tarehe 30/01/2018 kikao hiki kinatajiwa kijielekeza katika kujadili majibu ya Hoja za vyama vya siasa na kutoa majibu kwa maoni/mapendekezo yaliyojitokeza wakati wa kujadili taarifa ya Kamati ya Fedha pamoja na ile ya Ushauri ya Wilaya na kisha Baraza hili ambalo ndio chombo cha juu cha maamuzi katika Halmashauri linatarajiwa kupitisha kifungu kwa kifungu Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya hii Bajeti ya kiasi cha Tsh. 42,465,119,022.94 iliyotengwa kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 kwa ajili ya kufikia vipaumbele kadhaa vilivyowekwa katika mpango wa Bajeti kwa mwaka huu.
Kupitishwa kwa Bajeti hii katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya kunatarajiwa kuruhusu kufanyika kwa vikao mbalimbali vya ngazi ya mkoa kabla ya kupitishwa rasmi na Bunge na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye kikao chake cha Bajeti kinachotarajiwa kuketi mapema kuanzia mwezi Aprili mwaka huu mjini Dodoma. Vikao vingine vinavyotajiwa kujadili mapendekezo ya Mpango huu wa Bajeti ni kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) kinachotarajiwa kukutana mjini Bukoba mnamo Februari Mosi, 2018.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.