Agizo la Rais Magufuli Lakutoa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Walemavu Laendelea Kutekelezwa Wilayani hapa.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imeendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alililitoa mwezi Novemba, 2015 alipozindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma na kisha kulirudia mara kadhaa kuhusu Halmashauri zote nchini kutenga kiasi cha asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na wanalemavu ambapo katika kipindi cha mwezi Oktoba mpaka Desemba 2017, Halmashauri hii imetenga jumla ya shilingi 60,800,000 kwa ajili ya vikundi 33 kwa ajili ya utoaji wa mikopo hiyo.
Zoezi hilo ambalo lilikuwa limeambatana na shamrashamra za aina yake lilifanyika katika viwanja vya kituo Rafiki cha Vijana cha Angaza mnamo 26/01/2018.
Mapema, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Wilayani hapa Bi. Adeodata A. Peter katika taarifa iliyosomwa nae kwa mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Geofrey Mheleuka alielezea kwamba Halmashauri ya Wilaya hii imekuwa na desturi ya kutoa mikopo kwa SACCOS na vikundi vya wanawake na vijana tangu mwaka 1998 na kwamba vikundi hivyo vimeshanufaika kwa kuboresha miradi yao ambayo imewapelekea kujiinua kiuchuni na kuboresha hali zao za maisha na pia kuwaongezea ajira wanawake na vijana.
“Mh. Mgeni rasmi kumbukumbu zinaonesha kwamba kwa mwaka 2015/2016 Jumla ya Sh. 125,188,000 zilitolewa kwa vikundi 41 na SACCOSS 03 ambapo kati ya fedha hizo 28,000,000 ni kutoka Wizara ya Sera, Bunge, Vijana na Walemavu na Sh. 97,188,000 zilitokana na mzunguko wa wanawake na vijana utokanao na mapato ya ndani”, ilibanishwa kupitia taarifa hiyo iliyosomwa na Bi. Adeodata.
Aidha taarifa hiyo iliendelea kubainisha kwamba kwa mwaka 2016/2017 jumla ya Sh.196,000,000 jumla ya vikundi 103 vya wanawake na vijana viliweza kunufaika.
“Kwa robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba 2017 jumla ya Sh.18,000,000 zimetolewa kwa vikundi 06 kutoka kata 06 sambamba na jumla ya 15,506,913.98 zilizohamishwa kutoka mapato ya ndani kwenda mfuko wa wanawake na vijana ikiwa ni sehemu ya asilimia 10 kwa miezi ya Julai na Agosti 2017”, ilisisitiza taarifa hiyo.
Aidha kupitia taarifa yake hiyo Bi. Adeodata alibainisha baadhi changamoto zinazokabili zoezi la utoaji wa mikopo kwa makundi hayo ambapo alitaja baadhi ya vikundi kutokurejesha mikopo hiyo kwa wakati kwa mujibu wa mkataba huku akiitaja changamoto hii kuligusa sana kundi la vijana.
“Mh. Mgeni rasmi changamoto nyingine ni mtaji usiotosheleza mahitaji ya waombaji wa mikopo pamoja na upungufu wa vitendea kazi kwa ajili ya kufuatilia vikundi vilivyopewa mikopo”, alisisitiza Bi.Adeodata.
Kupitia taarifa hiyo Bi. Adeodata alitaja baadhi ya mambo yaliyosaidia katika utatuzi wa changamoto hizo ikiwemo kumshirikisha Mkuu wa Wilaya kwa baadhi ya vikundi vinavyoshindwa kurejesha mikopo hiyo na kwa wakati lakini pale wanaposhindwa kufanikiwa kupata ufumbuzi kuvipeleka vikundi hivyo mahakamani.
Changamoto nyingine zilizotajwa kupitia taarifa hiyo zilikuwa ni kiasi kidogo cha fedha huku utatuzi ukitajwa kwamba kiasi hicho kilichopo kimekuwa kikigawanywa kwa uwiano sawa kwa kata zote.
“Aidha raslimali kidogo zilizopo zimekuwa zikitumika katika shughuli za ufuatiliaji na zaidi tumejitahidi kuendela kutoa Elimu kwa vikundi hivi vya mikopo”, alisisitiza Bi. Adeodata.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mh. Mheluka aliupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya kwa kutekeza agizo la serikali la kutenga Fedha hizo na kuzitoa huku akisisitiza kwamba Halmashauri zote zimekuwa zikitenga Fedha hizo lakini Halmashauri chache ndizo zimekuwa zikitekeleza agizo hilo kwa vitendo.
“Lakini pamoja na hayo yote niendelee kuwasisitiza uongozi wa Halmashauri kwamba kabla ya kukimbilia mahakamani kwa ajili ya kuvishtaki vikundi hivyo ambavyo vinashindwa kurejesha mikopo yao, uongozi wa Halmashauri hauna budi kuwasiliana kwanza na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kabla ya kwenda mahakamani ambapo kesi hizo hutumia muda mrefu”, alisisitiza Mkuu wa Wilaya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mh. Wallace Mashanda na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya, Mh. Robinson Mutafungwa wote kwa pamoja walipongeza hatua hiyo lakini wakalisihi kundi la vijana kuiga mfano kutoka kwa kundi la wanawake juu ya nidhamu ya urejeshwaji wa mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya Karagwe aliweza kukichangia kiasi cha Sh.1,000,000 kikundi cha Jumuishi ambacho ni kikundi cha walemavu ili kuweza kukiongezea nguvu zaidi katika kujikwamua kiuchumi.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.