VIJIJI TAKRIBANI 40 KUPATA UMEME KUPITIA REA III
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Medard Kalemani amezindua mradi wa usambazaji wa umeme vijijini, REA awamu ya tatu wilayani hapa ambapo mradi huu unaenda kutekelezwa katika takribani vijiji 40 ikiwa ni ongezeko la vijiji 19 kwenye orodha ya vijiji 21 vilivyokuwa vimeainishwa hapo awali.
Katika tukio hilo la uzinduzi ambalo lilifanyika katika kijiji cha Katanda kilichopo katika kata ya Kihanga, Mh. Dtk Kalemani alitumia mkutano huo uliokuwa umefurika umati wa wananchi kutoka katika kila pembe ya kata ya Kihanga na maeneo mengine ya Wilaya ya Karagwe kutoa maelekezo na maagizo mazito kwa viongozi wa REA na wale wa Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO wa Wilaya na Mkoa kwa ujumla.
Baadhi ya maelekezo na maagizo hayo yalikuwa ni kuhakikisha katika utekelezaji wa mradi huu wa REA III watendaji hao wahakikishe ya kwamba hakuna kaya inayorukwa bila kuwekewa umeme kwa kisingizio cha kwamba nyumba ya kaya hiyo sio bora huku akionya vikali ya kwamba kiongozi yeyote atakayekwenda kinyume na agizo hilo atawajibishwa bila kuonewa haya.
“Hatuna shida ya umeme hapa nchini, tatizo kubwa katika sekta hii ni kwamba kuna hujuma kwenye miundombinu na hii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na wananchi wenyewe wanaohujumu miundombinu hiyo na nitoe wito kwenu kuilinda miundombinu hiyo na kuwafichua wote wanaohusika na hujuma hiyo kwenye mamlaka zinazohusika”, alisisitiza Waziri Kalemani.
Maagizo na maelekezo mengine aliyoyatoa Waziri huyo kwa watendaji na wakandarasi na watendaji wa REA na TANESCO lilikuwa ni suala la kuhakikisha wanawaunganishia umeme wananchi ndani ya siku saba kutoka wanapolipia na kutoa agizo kali kwa watendaji hao kuhakikisha wanawaunganishia umeme wananchi wote ambao walishalipia gharama za uunganishaji wa huduma hiyo pasipo kuunganishia kwa muda mrefu huku agizo hilo likitakiwa kutekelezwa kabla ya Julai, 01 mwaka huu.
Aidha katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alitoa wito kwa mamlaka zote za taasisi za serikali kuhakikisha wanaweka mikakati ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya taasisi hizo kama vile vituo vya kutolea huduma za afya na shule kufikiwa na huduma hiyo ya umeme huku akiahidi ya kwamba oparesheni itafanyika katika taasisi hizo ili kubaini juu ya utekelezwaji wa jambo hilo ikiwemo kujua sababu za kushindwa kutekelezwa kwa jambo hilo.
Awali Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Mh. Innocent Bashungwa licha ya kumshukuru waziri Kalemani kwa uchapakazi wake huku akinainisha ya kwamba hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa waziri huyo kuzuru wilaya ya Karagwe kwa kipindi cha takribani miaka miwili na nusu, alimweleza waziri huyo juu ya uwepo wa suala la rushwa wakati wa utekelezaji wa mradi wa REA II ambapo lugha maarufu ya Jiongeze upate umeme iliyokuwa na lengo la kuwashawishi wananchi kutoa fedha kwa ajili ya kufanikisha kupata huduma hiyo ya umeme ilitawaka katika kipindi hicho.
Katika kujibu hoja hiyo, Waziri Kalemani alimwagiza Mkuu wa Wilaya Karagwe na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kujipanga na kuhakikisha jambo hilo halijirudia tena huku akitoa wito kwa watendaji wa REA, TANESCO na wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa na kuepuka vitendo hivyo.
Aidha katika kusisitiza jambo hilo, Waziri Kalemani alisema gharama ya kuunganishia umeme ni sh. 27,000/= tu ambapo hata hivyo aliagiza uwepo utaratibu wa wananchi kulipa kidogo kidogo kwa fedha hiyo na wanapokamilisha ulipaji wa fedha hiyo waunganishiwe huduma hiyo ndani ya muda wa siku saba.
Katika hatua nyingine na kupitia mkutano huo, waziri Kalemani aliweza kugawa vifaa takribani 250 vilijulikanavyo kama umeme tayati (UMETA) ambavyo hazihitaji kufungwa kwa mifumo ya nyaya za umeme katika utoaji wake wa huduma ya umeme ambapo kwa wale wanaohitaji vifaa hivyo watapaswa kununua kwa bei isiyozidi kiasi cha shilingi 36,000/=
Mkutano huu ulimalizika huku Mwenyekiti wa kijiji cha Katanda, Protace Matabaro akimshukuru sana waziri Kalemani kwa kufanya ziara kama hiyo kijijini hapo na zaidi akiipongeza mipango ya wizara Nishati katika kuhakikisha wananchi wa vijijini ikiwemo kijiji cha Katanda wanafikiwa na huduma hiyo muhimu katika kufikia maendeleo ya viwanda.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.