PS3, TAMISEMI Wafika Wilayani Karagwe kwa ajili ya Kuboresha Mifumo ya Mawasiliano.
Na Innocent E. Mwalo, Karagwe.
Timu ya Wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI pamoja na wataalam wengine kutoka Shirika linalojishughulisha na uimarishaji wa mifumo katika sekta ya Umma, PS3 mnamo Januari 23, 2018 wamefika Wilayani hapa kwa ajili ya kuona namna mifumo ya mawasiliano ya kompyuta inavyofanya kazi wilayani hapa na kusaidia kutatua changamoto hizo za kimifumo.
Ujumbe huo uliokuwa na jumla ya wataalam sita (06) uliwahusisha ndugu Jeremia Mtawa, ndugu Jonas Kiluwa, ndugu Amri Kamugisha na ndugu Victor Msama.
Wengine katika ujumbe huo walikuwa ndugu Henry Shishira na ndugu Doris Christopher ambapo mara baada ya ujumbe huu kuwasili ulikwenda moja kwa moja ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hii ndugu Godwin Kitonka.
Wataalam kutoka Halmashauri hapa walikuwa ndugu Reginald Kiwango, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji Wilayani na Beatus Nyarugenda, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA.
Awali ya yote ndugu Kitonka aliwashukuru sana wataalam hawa kwa kufika wilayani hapa kwa lengo la kubadilishana uzoefu na wataalam wa Halmashauri ya wilaya hii na kuwaomba wakague mifumo yote ya mawasiliano na kutoa mapendekezo na ushauri huku akiahidi menejimenti kuyafanyia kazi mapendekezo yote yatakayotolewa baada ya ukaguzi huo.
“Napenda kuwahakikishia kwamba Halmashauri ya Wilaya Karagwe inatambua umuhimu wa uimarishwaji wa mifumo ya mawasiliano na bila ya kuyapokea maelekezo na ushauri wenu tunaweza tusifanikiwe katika utendaji kazi wetu ambao kwa kiasi kikubwa sana unategemea mawasiliano ya hayo”, alisikika ndugu Kitonka
Kisha baada ya mazungumzo hayo wataalam hawa walipata nafasi ya kukagua mifumo kadhaa ya kielekroniki ikiwemo tovuti ya Halmashamauri ya Wilaya Karagwe, mfumo wa malipo(FFARS), Mfumo wa Mapato (LGRCIS) na Mfumo wa Malipo kwenye Kituo cha Afya cha Kayanga (HOT BEMIS).
Mara baada ya ukaguzi wao wataalam hawa walipongeza jitihada kadhaa za Halmashauri ya Wilaya katika matumizi ya Mifumo hii lakini wakatoa mapendekezo kadhaa ikiwemo suala la kununua vifaa ili kukabiliana na changamoto ya kukosekana kwa vitendea kazi kama vile kompyuta lililojitokeza kwenye baadhi ya maeneo wakati wa ukaguzi wao.
Aidha kupitia taarifa yao ya ukaguzi waliweza kuainisha changamoto nyingine ya baadhi ya wataalam hasa kwenye vituo vya Afya, zahanati na shule kushindwa kuutumia mfumo wa malipo wa FFARS.
Changamoto nyingine iliyowasilishwa kupitia taarifa yao ilikuwa ni ukosefu wa mashine za kukusanyia mapato (POS) ambapo kupitia taarifa hiyo walibainisha upungufu wa mashine takribani 60.
Aidha wataalam hawa walishauri Afisa TEHAMA wa Wilaya, Mkaguzi wa Ndani na Afisa Mapato kushirikiana katika kufanya ukaguzi ili kuweza kuondoa kasoro zilizojitokeza katika ukaguzi wa mashine hizi ikiwemo suala la kukosekana kwa usuluhishi wa mapato kwenye mashine hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya aliishukuru timu hiyo ya wataalam na kuahidi kuyafanyia kazi mapungufu hayo kama yaliyoibuliwa na wataalam hao kupitia taarifa yao ya ukaguzi.
“Kama nilivyosema hapo awali kwamba fanyeni ukaguzi wenu bila kutupendelea ili kupitia mapungufu mtakayoyaibua tuweze kufanya vizuri sana”, alisisitiza ndugu Kitonka.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.