“Ni lazima tufike asilimia 100 chanjo ya Watoto Wilayani Karagwe”, asema Mheluka
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Mkuu wa Wilaya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Msingi ya Afya (PHC) wilayani hapa na wajumbe wote wa Kamati hiyo Ijumaa ya tarehe 15 Septemba, 2017 kwa kauli moja waliweka azimio kwamba Halmashauri ya wilaya hii na uongozi wa wilaya kwa ujumla ufanyie kazi changamoto zote zilizoibuliwa na Idara ya Afya chini ya Mganga Mkuu wa Halmashahuri ya wilaya hii, Dkt. Libamba Sobo kupitia taarifa yake ya utekelezaji wa shughuli za Kitengo cha chanjo kwa kipindi cha Januari- Juni 2017 ili kuhakikisha wilaya inafikia lengo lake la kutoa chanjo kwa watoto kwa asilimia 100.
Awali katika taarifa hiyo iliyosomwa na Bi. Modesta Kibona ambaye ni Mratibu wa Huduma za chanjo wilayani hapa kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya, ilianisha changamoto kadhaa zinazowakabili wataalam wa Idara ya Afya wakati wa utoaji wa chanjo hizo ambazo zinasaidia kukinga magonjwa anuai kama vile polio(kupooza ghafla), Kifua kikuu, Homa ya ini, Dondakoo, Pepopunda, Kifaduro, Homa ya Uti wa mgongo, Kichomi, Kuhara, Surua, na Rubella.
Lakini pia taarifa hiyo iliitaja chanjo nyingine inayokusudiwa kuzuia kansa ya shingo ya kizazi kwa wasichana wa miaka 9- 14 ambapo kwa mujibu wa taarifa hiyo chanjo hiyo itaanza kutolewa nchini hivi karibuni.
Kwa hiyo Mh. Mheluka alisisitiza kupitia kikao hicho kuwa ni lazima Wilaya Karagwe izifanyie kazi chanagamoto zote zilizoibuliwa na wataalam wa Afya katika taarifa hiyo ya utekelezaji wa utoaji wa chanjo kwa watoto ili wilaya iweze kuvuka lile lengo kuchanja watoto hadi kufikia asilimia 95 kwa chanjo zote.
Kwa hiyo kupitia kikao hicho yaliwekwa maazimio na mikakati kadhaa ya kufanikisha jambo hilo.
Azimio la kwanza lilikuwa ni kwa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya kupitia ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba upungufu wa vyombo vya usafiri hususani pikipiki na boti unafanyiwa kazi haraka iwezekavyo ambapo Mganga Mkuu wa Wilaya aliagizwa kuandaa upya utaratibu wa ugawaji wa pikipiki ili ziweze kusambazwa hasa kwenye maeneo ambayo taarifa ya utekelezaji wa shughuli za chanjo ziliyataja kutokufanya vizuri kutokana na kutokufikiwa vizuri na usafiri wa magari kutokana na jiografia ya wilaya ya Karagwe.
Katika kujibu juu ya suala hili la ugawaji upya wa pikipiki, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Sobo alikiri kwamba ofisi yake ilishaliona tatizo hili na tayari lilishafanyia kazi kwa kupeleka pikipiki maeneo ya Chenjubu huko Ruhita ambapo kuna changamoto kubwa ya gari la chanjo kufika huko ili kuweza kusambaza chanjo hizo.
Mjadala ilikuwa mkali kwenye suala la usafiri wa boti ambapo baadhi ya wajumbe walielezea kwa masikitiko makubwa adha wanayopa wanapotekeleza shughuli zao sio tu za chanjo hata zile zinazohusu oparesheni na ukusanyaji wa mapato kwenye kutokana na kosekana kwa boti ya uhakika kwenye maeneo ya Nyakabanga, Ruhita na Chamchuzi ambapo washiriki walitoa rai ya kununuliwa kwa boti ya kisasa ili kuwaepusha na adha ambayo wakati mwingine huwalazimu kuvuka mto kwa kutumia boti zisizokuwa imara hali inayopelekea kuhatarisha maisha yao.
Kikao hicho tena kwa kauli moja kiliazimia kwa kumwagiza Afisa Mipango wa Wilaya, ndugu Herbert Bilia kuhakikisha anaushauri uongozi wa Halmashauri ya wilaya kutekeleza katika mipango ya awali suala la ununuzi wa boti kwani tayari katika bajeti ya mwaka wa Fedha 2017/2018.
Changamoto nyingine iliyojadiliwa sana ilikuwa ni suala la baadhi ya vijiji kutokuwalipa kwa kipindi kirefu wahudumu wa afya wa ngazi za vijiji ambapo vipo takribani 173 wanaofanya kazi mbalimbali za afya kwa kata zote 23 ambapo kila kijiji kinatakiwa kuwa na wahudumu wawili.
Azimio lililowekwa kwenye changamoto hii ilikuwa ni kwamba Mkuu wa Wilaya na watumishi wa Idara ya Afya waandae mikutano ya hadhara kwenye vijiji vilivyoshindwa kuwalipa wahudumu hawa wa Afya.
Lengo la mikutano hii ni kuwahamasisha wananchi ili wapate elimu ya umuhimu wa kuchangia gharama hizo na hivyo Katibu Tawala wilaya Mh. Innocent Nsena aliagizwa kusimamia suala la uratibu wa ratiba hiyo ya mikutano.
Changamoto nyingine ilikuwa ni suala la baadhi ya zahanati kutokujenga mabanda kwa ajili ya huduma za mkoba katika maeneo yao na kupelekea wateja kukosa huduma wakati wa mvua ambapo kikao kiliwaagiza maafisa Tarafa kwenda kwenye maeneo yao kuhamasisha ujenzi wa mabanda hayo na kikao kijacho iliamriwa itolewe taarifa ya utekelezaji wa jambo hili.
Ilitajwa changamoto nyingine ya migogoro ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Kashanda kuathiri suala hili la chanjo ambapo Mkuu wa Wilaya, Mh. Mheluka alikihakikishia kikao hicho kuwa jitihada kubwa zinafanywa kumaliza jambo hilo na akawahikikishia washiriki wa kikao hicho kwamba jambo hili halitakuwa changamoto tena wakati ujao.
Kuhusu changamoto ya wahamiaji wanaotoka nje ya wilaya Karagwe, Mh. Mheluka aliwahakikishia washiriki kuwa jambo hili litamalizwa kupitia usajili wa mamlaka ya vitambulisho vya Taifa ambapo watasajiliwa wanananchi wale wenye sifa tu.
Changamoto nyingine ilikuwa ni uchakavu wa majokofu ya chanjo na ukosefu wa vipuri toka ngazi ya Taifa ambapo Mtaalamu toka shirika la John Snow Inc (JSI), Nassor Mohamed ambao ni wabia wa serikali kwenye masuala ya afya ya chanjo aliahidi kwamba wao kwa kushirikiana na serikali wapo mbioni kumaliza tatizo hilo na baada ya muda mfupi kwa kuleta majokofu hayo na vipuri na akaahidi baada ya utekelezaji wa jambo tatizo hilo litabaki kama historia itabaki historia.
Changamoto nyingine zilizoibuliwa zilihusu Jamii kuwaficha watoto wanaopooza ghafla bila kuwaleta kwenye vituo vya tiba na akina mama kujifungulia majumbani na kuchelewesha watoto kupata chanjo ya polio ambayo hutolewa ndani ya siku 14 ambapo azimio liliwekwa kwamba Elimu itolewa kwa kupitia mikutano ya ngazi zote ili Jamii iweze kuelimishwa juu ya mambo hayo.
Suala jingine lililotajwa kukwaza utoaji wa chanjo lilikuwa ni ushiriki hafifu wa baadhi ya viongozi wa Kata, Vijiji na Vitongoji katika kuwatafuta watoto walio nyuma ya ratiba za chanjo ambapo iliamriwa Mkuu wa wilaya kupitia Mikutano yake ya hadhara aendelee kutoa Elimu hiyo.
Pamoja na changamoto zilizoainshwa hapo juu kwa kipindi cha Januari- Juni, 2017 Wilaya ya Karagwe imefanikiwa kuvuka lengo kwa kuwachanja watoto 6,934 kati ya 14,340 wanaotarajiwa kuchanjwa Penta 03 kwa mwaka 2017 ambapo kwa malengo yaliyowekwa na Idara ya Afya Wilayani hapa ni kuhakisha wanavuka asilimia 95 na kuvuka rekodi za mwaka jana 2016 ambapo takwimu za uchanjaji zinaonesha kwamba kiwango cha uchanjaji kilikuwa ni asilimia 91.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.