Mh, Tizeba: Marufuku Watu Binafsi Kununua Kahawa za Wakulima.
Na, Geofrey A. Kazaula – Karagwe.
Waziri Wa Kilimo na Ushirika Mh, Charles Tizeba ( Mb) ameendelea kukazia maagizo ya serikali kwamba ni marufuku watu binafsi kujihusisha na ununuzi wa Kahawa za wakulima iwe ni baada ya mavuno au kwa njia ya kienyeji maarufu kama “ Butula” na kwamba kahawa zote zitanunuliwa na vyama vya ushirika tu.
Kuhusu hatima ya watu walio kwisha nunua kahawa za wakulima kwa njia ya butula , Mh Waziri amefafanua kuwa watu hao wajiorodheshe katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kwamba watarejeshewa kiasi chao cha fedha kutoka kwa wakulima mara baada ya mauzo ya Kahawa ambayo yatafanyika kwa njia yamnada.
“ Mkulima atarejesha kiasi kilekile cha fedha alicho poakea kutoka kwa mnunuzi wa “butula” mfano, kama mtu alitoa fedha T.Sh 60,000 kwa gunia atarejeshewa kiasi hichohicho na mkulima baada ya kuuza kahawa yake” alisema Mh, Waziri.
Katika taarifa iliyotolewa na chama cha Ushirika Wilayani Karagwe KDCU wamebainisha kuwa kuna changamoto kwa baadhi ya watu kuwapotosha wakulima kuwa mfumo wa kuuza kahawa kupitia vyama vya ushirika utachelewesha malipo ya wakulima na kwamba wakulima watakopesha Kahawa kwa muda mrefu.
Mh, Waziri Tizeba amewataka wananchi kutupilia mbali upotoshwaji huo na kueleza kuwa Serikali inaandaa mpango na sheria ambapo mkulima atakapo kabidhi Kahawa yake kwa Chama cha Ushirika, chama kitampatia sehemu ya malipo yake kwa mujibu wa bei elekezi na malipo yaliyobaki atapewa baada ya Kahawa kuuzwa.
Aidha, Mh waziri amefafanua vizuri kuwa lengo la serikali si kuruhusu vyama vya ushirika kupanga bei na kumlipa mkulima na kisha kujipatia faida kama chama na kusema kuwa Kahawa ni mali ya Mkulima hadi inapofika mnadani na hivyo mkulima atanufaika na bei ya mnadani moja kwa moja tofauti na ilivyo kuwa zamani ambapo bei ya mwisho ililenga kukinufaisha chama cha Ushirika.
Wilaya ya Karagwe tayari ianvyo viwanda vya kukoboa kahawa, Mh, waziri amesisitiza kuwa lengo la Serikali si kufunga viwanda hivyo na kusema kuwa viwanda vitaendelea kukoboa kahawa ya mkulima na kulipwa na amesisitiza kuwa njia hiyo ikibainika inatumika vibaya kupitishia kahawa za “Butula”, sheria itachukua mkondo wake.
“ Wenye viwanda wataendelea kukoboa kahawa kwa kulipwa na ambaye ataona kufanya hivyo hanufaiki basi akalime kahawa zake auze.”
Kufuatia kauli hiyo, Mh Waziri pia ameagiza kufanyika kwa sensa ya wakulima wote, kila mtu anacho kilima, anacho kifuga , matarajio ya kuvuna na kwamba zao la kahawa pia kila mkulima awe anafahamika kiasi anacho kilima na makadilio yake ya kuvuna ili kila anayeuza kahawa awe anafahamika na kuondoa kasumba ya wasiolima kukutwa wanauza kahawa za wananchi na kujinufaisha huku mkulima akipata hasara.
Wilaya ya Karagwe ni miongoni mwa Wilaya zinazo zalisha kwa wingi zao la Kahawa ambapo wanachi wengi wamekuwa wakiuza kahawa zao kwa njia ya “Butula” na kuwanufaisha wafanya biashara wachache suala lililopelekea Serikali ya awamu ya tano kuweka mpango wa kuuza zao hilo kwa njia yamnada kupitia vyama vya ushirika ili Mkulima aweze kupata faida na haki yake moja kwa moja.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.